Hati ya Huruma
Kanuni ya huruma iko katika msingi wa dini zote, katika tamaduni za maadili na imani zinazotuhimiza tuwafanyie wenzetu wote jinsi sisi tunavyopenda tufanyiwe. Huruma hutuwajibisha tufanye bidii bila kuchoka ili kuwaondlea viumbe wenzetu dhiki na mateso, tusijiweke mbele katika maisha yetu bali tuwajali wenzetu kabla sisi wenyewe, na tuheshimu utakatifu mkuu wa kila mwanadamu, na bila kubagua tuhusiane na kila mtu kwa haki kamili, kwa usawa na kwa heshima.
Ni muhimu pia maishani tukiwa hadharani au tukiwa peke yetu tuwe na hisia za huruma na tuendelee kujizuia kusababisha mateso. Kufanya mambo au kuongea kwa hasira inayomletea mtu yoyote mateso, kudharau wanawake, au kujifikiria sisi tu, kusababisha umasikini, kudhulumu au kumnyima mtu yeyote haki msingi na kuzusha chuki kwa kudharau wengine ~ hata kama ni maadui wetu~ ni kwenda kinyume na uwanadamu wetu wa pamoja. Tunakubali kuwa hatujafaulu kuishi kwa moyo wa huruma na kwamba baadhi ya watu wametumia jina la dini na wakaongezea binadamu kiwango cha dhiki.
Kwa hivyo tunahimiza waume na wanawake wote ~ waifanye tena huruma iwe katika kiini cha desturi njema na dini ~ warudishe upya nguzo ya zamani ya kwamba ufafanuzi wowote wa maandishi ya dini ambao unazusha uhasama, chuki au dharau sio haki ~ wahakikishe kwamba vijana wanapewa maelezo ukweli tena ya kuheshimika kuhusu tamaduni, dini na mila nyengine ~ wahimize na watie mkazo kukubaliwa kwa moyo mkunjufu tofauti za tamaduni na dini ~ wakuze imani ya dhati kwa wanadamu wote wanaoteseka ~ hata wale wanaosemekana kuwa maadui.
Ni muhimu sana tuifanye huruma iwe nguzo dhahiri, yenye mwangaza tena iliyo imara katika hii dunia yetu iliyo na migawanyiko. Kwa sababu ya msingi wake wa kanuni ya kujibidiisha kuwachana na uchoyo, huruma inaweza kuangamiza mipaka ya kisiasa, ya kifikra, ya sera na ya kidini. Kwa kuwa inatokana na kutegemeana kwetu pamoja, huruma ni muhimu katika uhusiano wa wanadamu na kwa jumuiya ya kibinadamu inayotosheka. Ni njia ya kufikia kuelimika kwa hali ya juu, na pia ni kiungo muhimu kabisa katika kubuni uchumi wa haki na jumuiya ya ulimwengu yenye amani.